HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, December 8, 2017

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAPUNGUA HADI ASILIMIA 4.4

Na Emmanuel Ghula
Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Novemba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 4.4 kutoka asilimia 5.1 mwezi Oktoba, 2017. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma mbalimabli kwa mwezi Novemba, 2017.

“Mfumuko wa Bei wa mwezi Novemba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 4.4 kutoka asilimia 5.1 kwa mwezi uliopita wa Octoba, 2017. Hii imechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kama vile nyama ya ngombe ambayo imepungua kwa asilimia 5.4, samaki wabichi kwa asilimia 22.2, mbogamboga kwa asilimia 3.9, viazi mviringo kwa asilimia 14.0, mihogo mibichi kwa asilimia 24.8 na viazi vitamu kwa asilimia 13.4,” amesema Kwesigabo.

Amesema fahirisi za bei zimeongezeka hadi 108.94 mwezi Novemba, 2017 kutoka 108.41 mwezi Oktoba, 2017.

Kwesigabo amesema mfumuko wa bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Novemba, 2017 umepungua hadi asilimia 4.73 kutoka asilimia 5.72 mwezi Oktoba, 2017 na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 4.0 mwezi Novemba, 2017 kutoka asilimia 4.8 mwezi Oktoba, 2017. 

Amesema  bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na mafuta ya taa yaliyoongezeka kwa asilimia 4.6, mafuta ya dizeli kwa asilimia 2.0 na mafuta ya petrol kwa asilimia 2.8. 

Amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 91 na senti 79 mwezi Novemba, 2017 ikilinganishwa na Shilingi 92 na senti 25 ilivyokuwa mwezi Oktoba, 2017.
 Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza mfumuko wa bei wa Taifa wa mwezi Novemba, 2017.
Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki katika mkutano wa kutangazwa kwa mfumuko wa bei wa Taifa leo jijini Dar es Salaam katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA)


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad