HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 28 November 2017

ZAHANATI SITA ZASHINDWA KUTOA HUDUMA MOROGORO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Ngerengere, Bi. Kibena Nassoro akizungumza.

ZAHANATI sita zilizokamilika zote zikiwa Wilayani Morogoro Vijijini zimeshindwa kuanza kutoa huduma za afya na kubaki mithili ya magofu baada ya kukosekana kwa watumishi watakaofanya kazi katika zahanati hizo.

Zahanati hizo ambazo zimekamilika kabisa na zipo tayari kuanza kazi ya kutoa huduma kwa wananchi ni pamoja na Zahanati ya Dakawa, Zahanati ya Singisa, Zahanati ya Tununguo, Zahanati ya Selembale, Zahanati ya Bamba na Zahanati ya Maseyu.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam kwenye semina iliyoandaliwa na TGNP Mtandao kwa baadhi ya wenyeviti wa halmashauri pamoja na mameya lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja changamoto anuai zinazoukumba mchakato wa bajati tangu ngazi za mitaa na vijiji, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Bi. Kibena Nassoro alisema zahanati hizo licha ya kukamilika zimeshindwa kutoa huduma baada ya kukosekana kwa wahudumu wa afya.

Bi. Kibena Nassoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngerengere, alisema awali walifikiria kuwatawanya watumishi idara ya afya walionao eneo hilo ili kuhakikisha zahanati hizo zinaanza kazi lakini zoezi la kusaka vyeti feki lililofanywa na Serikali liliathiri mipango hiyo maana lilifukuza watumishi 23 katika idara hiyo.

Alisema mahitaji halisi ya watumishi idara ya afya katika halmashauri hiyo ni 511 na waliopo kwa sasa ni 326, huku katika zoezi la kubaini vyeti feki likiathiri wafanyakazi 23 kwenye idara hiyo hali iliyoongeza changamoto katika idara hiyo.

Awali tulifikiria kuwagawanya hawa kwa kujibana ilimradi zahanati zetu zianze kutoa huduma kwa kujibana, lakini zoezi la kusaka vyeti feki lilileta changamoto zaidi...maana walipungua na sehemu nyingine zilizokuwa zikitoa huduma kukosa kabisa hivyo tumewagawa na kuna maeneo mengine unakuta tuna daktari na nesi mmoja tu wakitoa huduma...," alisema Bi. Kibena.

Aliongeza kuwa zoezi la kuzifunga kutoa huduma zahanati zilizokamilika katika halmashauri hiyo huwenda likazikumba tena zahanati za Ledewa na Zahanati ya Lubasazi ambazo zipo katika hatua za mwisho kukamilika kwenye ujenzi wake. Aliongeza kuwa tayari wamekwisha kuomba watumishi wa idara hiyo mamlaka husika ili kukabiliana na changamoto inayowakabili kwa sasa.

Imeandaliwa: www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad