HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 30, 2017

WAKIMBIZI NCHINI TANZANIA NA RWANDA WAPATIWA MSAADA MUHIMU NA UJERUMANI

 DAR ES SALAAM – Serikali ya Jamhuri ya Kifederali ya Ujerumani imetoa mchango wa Euro milioni 2 kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani  (WFP) ili taasisi hiyo imudu kuendelea kutoa msaada wa chakula kwa takribani nusu milioni ya wakimbizi na watu wanao omba hifadhi waishio katika nchi za Tanzania na Rwanda. Mchango huu wa fedha ni muhimu sana kwa kazi za kuhudumia wakimbizi zinazofanywa na WFP katika ukanda huu ambapo shirika hilo linakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha. Kutoka katika mchango huo, kazi za WFP katika nchi za Tanzania na Rwanda kila moja itapokea Euro milioni 1. Balozi wa Ujerumani Detlef  Wächter alisisitiza  umuhimu wa kuwepo kwa msaada wa haraka kutoka jumuiya za kimataifa ili kupunguza makali ya changamoto za wakimbizi nchini Tanzania. 

“Tukiwa miongoni mwa wahisani wakubwa kabisa wa kimataifa, ni wajibu wa nchi yetu kusaidia na kuunga mkono juhudi za nchi wenyeji na mashirika ya kimataifa katika mgogoro huu wa kiutu. Tuna imani kwamba msaada huu wa fedha utaisaidia WFP kukabiliana na upungufu wa fedha uliopo hivi sasa.” Nchini Tanzania, mchango wa Ujerumani ulitumika kununua mahindi ambayo ni sehemu ya mgao wa kila mwezi wa chakula unaojumuisha pia kunde, chumvi, mafuta ya kupika na unga wa uji ulioongezwa virutubisho. Nchini Rwanda, mchango huo ulitumika hasa kununua mahindi na maharage kwa migao ya chakula cha kila mwezi. Vilevile, WFP Rwanda ilinunua unga wa uji ulioongezwa virutubisho, sukari na maziwa ya unga yenye viturubisho ili kuwasaidia watu walio katika hali mbaya zaidi wanaohitaji mlo maalumu.  
 Katika nchi zote mbili, WFP inatoa chakula cha nyongeza kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wagonjwa waliolazwa hospitalini na watu walio katika tiba ya VVU/UKIMWI na kifua kikuu. Programu hizi maalumu zinazolenga makundi ya watu hutoa lishe inayohitajika sana kupitia chakula cha ziada kama vile uji ulioongezewa virutubisho na maziwa ya unga yenye virutubisho. Vyakula hivi ni muhimu katika kukabiliana na tatizo la kudumaa na ukosefu wa lishe kwa watoto, na vinaongeza kinga ya mwili kwa watu walio na hali mbaya. Vilevile, WFP hutoa milo ya chakuala kilicho pikwa kwa wakimbizi walio katika vituo vya mpakani wakisubiri utaratibu wa kupokelewa.

“WFP inatoa shukrani za dhati kwa Ujerumani, ambayo katika miaka mitano iliyopita imekuwa miongoni mwa wahisani wetu wakubwa kabisa na imeimarisha zaidi utayari wake katika kutatua migogoro ya kiutu nchini Tanzania, ukanda na kote duniani,” alisema Mwakilishi wa WFP Tanzania Michael Dunford. “Mwendelezo wa msaada huu kutoka Ujerumani ni muhimu katika kukidhi mahitaji ya chakula kwa wanaume, wanawake na watoto waliokimbia makwao.” Tangu kuibuka kwa mgogoro nchini Burundi mwaka 2015, zaidi ya wakimbizi 258,000 kutoka Burundi waliingia nchini Tanzania, jambo lililoifanya Tanzania kuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kutoka Burundi katika ukanda wa Afrika Mashariki. 
Hivi sasa, Tanzania inawahifadhi takribani wakimbizi 317,000 katika kambi tatu, idadi ambayo ni takribani mara tano ya ile iliyokuwepo miaka miwili iliyopita. Kwa upande wake, Rwanda hivi sasa inawahifadhi wakimbizi 172,000 katika kambi sita. Katika hao, wakimbizi 87,000 wanatoka Burundi, ambapo 55,000 wanaishi katika Kambi ya Mahama na ambao wanategemea kwa asilimia zote msaada ili wajikimu katika mahitaji ya chakula. “WFP inaweza kuendelea kutoa chakula kwa watoto na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika kambi za wakimbizi, na hii ni kwa sababu ya msaada kutoka Ujerumani,” alisema Jean-Pierre de Margerie, Mkurugenzi na Mwakilishi wa WFP Rwanda. 
“Kwa kuwa wakimbizi wana nafasi ndogo ya kujiingizia kipato nchini Rwanda, msaada wa chakula unabaki kuwa wa muhimu sana.” Kufuatia mmiminiko mkubwa wa watu katika nchi zote hizi mbili, WFP linahitaji rasilimali zaidi ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi hasa yale ya msingi ya chakula. Tangu Februari, kutokana na kupungua kwa upatikanaji wa fedha, WFP nchini Tanzania ililazimika kupunguza mgao wa chakula hadi kufikia asilima 72 ya kiwango cha chini cha kalori 2,100 zinazohitajika.
Ili kurejesha mgao katika kiwango kinachostahili cha mahitaji ya chakula ya wakimbizi katika nchi zote mbili, WFP inahitaji nyongeza ya Dola za Marekani milioni 29 katika kazi zake nchini Tanzania na Dola za Marekani milioni 10 huko Rwanda kati ya sasa na mwezi Aprili, 2018. Endapo fedha za nyongeza hazitapatikana, huenda WFP ikalazimika kupunguza zaidi mgao wa chakula .

WFP ni shirika kubwa zaidi duniani la misaada ya kiutu linalopambana na njaa kote duniani, kutoa msaada wa chakula katika nyakati za dharura na linaloshirikiana na jamii ili kuinua viwango vya lishe na kujenga uwezo wa kujinusuru na majanga. Kila mwaka, WFP inawasaida takribani watu milioni 80 katika nchi 80 kote duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad