HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 16, 2017

SERIKALI KUENDELEA KUTOA ELIMU UFANYAJI KILIMO BORA CHA MBOGAMBOGA

 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Juma Aweso

Na Beatrice Lyimo, MAELEZO, DODOMA
Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji wa mbogamboga katika maeneo sahihi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Juma Aweso wakati akijibu swali la Mhe. Zainabu Amiri kuhusu Mpango wa Serikali wa kuwapatia maji safi na salama wakulima hao wa mbogamboga.

Mhe. Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji kwa kuzingatia umuhimu wa afya za wananchi inaendelea kutoa miongozo na ushauri kuhusu maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu na kwa shughuli za uchumi.

" Katika kuhakikisha wananchi wanalima mbogamboga katika maeneo sahihi, Serikali iliunda kikosi kazi kwa kushirikisha maafisa wa Baraza la Mazingira la Taifa(NEMC) ambapo kilitembelea baadhi ya mito ya Dar es salaam na kugundua uchafuzi mkubwa wa mazingira unaosababishwa na utiririshaji wa majitaka kutoka majumbani na kwenye viwanda ambapo maji hayo kuwa na kemikali zisizofaa kwa matumizi ya kilimo cha mbogamboga kwa mfano mto Msimbazi" amesema Mhe. Aweso.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema kuwa, Serikali inawataka wananchi kuacha kulima mbogamboga katika maeneo hayo yenye uchafuzi kwa kuwa maji hayo yana athari kwa afya.

Vilevile amesema kuwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) inaendelea kupima maji ya mito hiyo na kutoa taarifa za hali ya maji hayo.

Mbali na hayo, Mhe. Aweso ameshauri Halmashauri za Manispaa katika Jiji la Dar es Salaam kutunga na kusimamia Sheria ndogo kwa ajili ya kudhibiti uchafuzi wa maji ya mito hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad