HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 23, 2017

RAIA WAWILI WA SOMALIA NA MTANZANIA KIZIMBANI KWA UCHUMI

 Na Karama Kenyunko, Blogu ya Jamii.

RAIA wawili wa Somalia na Mtanzania mmoja, leo Novemba 23, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi na kuisababisha serikali  hasara ya Sh milioni 370.1.

Wakili wa serikali Jehovaness Zacharia amewataja washitakiwa hao kuwa ni, Mahad Ahmad Salat (30) mfanyabiashara na Mkazi wa Temeke,  Faudhia Abdi (31) mfanyakazi wa ndani na Ally Yusuf (22) Mwanafunzi na Mkazi wa Temeke.

Washtakiwa hao wamesomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Wakili Jehovanes amedai Agosti, mwaka huu  jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Salat aliingiza vifaa vya kielektroniki nchini pasipo kuwa na leseni kinyume na sheria.

Alidai washitakiwa hao waliingiza vifaa viwili vya mawasiliano ya Kimataifa vyenye namba za utambulisho DB 17-5060-1400=0269 na DB 27-6220-1860-0023 bila kuwa na leseni  kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Pia alidai kabla ya Agosti 25, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Salat aliunganisha vifaa viwili mawasiliano vya kielektroniki bila kuwa na leseni  ya TCRA.

Aidha katika shtaka la tatu, alidai washitakiwa wote kwa pamoja kati ya Agosti 25, na Oktoba 31, mwaka huu, Dar es Salaam, waliendesha mitambo ya mawasiliano ya Kimataifa kwa ajili ya kupokea mawasiliano bila kuwa na leseni.

Zacharia alidai kati ya Agosti 25 na Oktoba 31, mwaka huu jijini  Dar es Salaam, washtakiwa walikwepa kufanya malipo ambayo yalipaswa kufanyika kwa kuruhusu mawasiliano nje ya nchi kutokana na kutumia kifaa hicho cha mawasiliano bila kuwa na leseni.

Aidha, Washtakiwa kinyume na sheria walitumia vifaa vya mawasiliano vilivyounganishwa na vifaa vingine vya mawasiliano kwa nia ya kupokea mawasiliano bila kupata uthibitisho kutoka TCRA.

Washitakiwa hao wanadaiwa katika tarehe hizo wakiwa maeneo ya Temeke jijini Dar es Salaam  wakiwa wanaendesha mitambo bila leseni kwa pamoja waliisababishia TCRA hasara ya Sh 307,137,600.

Hata hivyo washitakiwa hawaruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza mashitaka ya uhujumu uchumi

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko alidai kuwa wanauhakika kwamba asilimia 80 upelelezi katika  mashitaka hayo umekamilika kwa kuwa haiwezekani kujua gharama zilizotokana na vifaa hivyo bila kufanya upelelezi. 

Alidai ni rai yao upelelezi huo ukamilishwe ili hadithi ya upelelezi isiendelee hadi mwakani.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 6, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad