HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 25, 2017

KINANA ASEMA HAKUNA WAZIRI WA KUKATAA ANALOMTUMA

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema hakuna waziri mwenye ubavu wa kukataa akimtuma jambo.

Amesema hayo jana Ijumaa Novemba 24,2017 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Moita Bwawani akimnadi mgombea wa CCM wa Kata ya Moita wilaya ya Monduli, Prosper Damuni.

"CCM ndiyo chama kilichoshika dola kama kuna changamoto sehemu yoyote namwambia waziri anayehusika anafika haraka eneo hilo kusikiliza na kutatua changamoto hiyo, hakuna waziri mwenye ubavu wa kukataa nikimtuma," alisema Kinana.

Katibu mkuu huyo amewaomba wananchi katika kata 43 zinazofanya uchaguzi mdogo wa udiwani kuwachagua wagombea wa CCM akisema ndicho chama kinachoongoza dola na ahadi zinazotolewa zinatekelezeka.

Kinana amewaomba wananchi hao akisema ni wakati muafaka kwao kuacha kupiga kura kwa ushabiki.

Alisema wilaya hiyo inakusanya mapato ya ndani ya Sh2 bilioni kwa mwaka wakati bajeti yao kwa mwaka ni Sh49 bilioni kwa mwaka fedha ambazo zinatolewa na Serikali Kuu hivyo ni muhimu kuwa na diwani anayetoka chama hicho ili kurahisisha maendeleo ya wananchi.

Kinana alisema anafahamu wilaya hiyo ina changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kutatuliwa.

"Nataka nimpe mbinu mgombea wenu akichaguliwa anatakiwa kuwa karibu sana na mkurugenzi mtendaji wa wilaya na kwa kuwa anatokana na CCM atakuwa na uwezo wa kuingia na kutoka kwenye ofisi za Serikali kutafuta fedha za maji, barabara, afya na elimu hiyo ndiyo kazi ya diwani si kukaa tu kusubiri maendeleo yaje," alisema Kinana

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa mikoa, Mrisho Gambo wa Arusha na Christopher ole Sendeka wa Njombe waliwataka wananchi kutoyumbishwa na kelele za vyama vingine bali wamchague mgombea wa CCM.

Mgombea udiwani, Damuni aliwaomba wananchi kumchagua ili alete maendeleo kwa kuzingatia chama chake ndicho kinachotekeleza ilani ya uchaguzi iliyoshinda mwaka 2015 na kuunda Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad