HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 14 November 2017

AZAM FC KUSHUSHA VIFAA VIWILI, KUSAJILI KUZIBA PENGO LA YAHYA MOHAMED


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
UONGOZI wa klabu ya Azam umepanga kufanya usajili wa mchezaji mmoja wa kigeni kutoka katika nchi za  Ghana na Zambia ambapo wanatarajia kushusha wawili ili kupata straika mmoja kati yai atakayemrithi Yahaya Mohamed.


Mapema mwezi huu, uongozi wa timu hiyo ulivunja mkataba na mshambuliaji wake Yahaya Mohammed ukiwa unakaribia mwaka mmoja tangu alipojiunga na timu hiyo kwa kile kinachodaiwa ni kushindwa kuonyesha kiwango kizuri tangu ajiunge na timu hiyo.


Azam FC imefikia makubaliano ya pamoja na mchezaji huyo raia wa Ghana na tayari wamemkabidhi barua ya kumruhusu kuondoka klabuni hapo.


Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba, wiki ijayo uongozi wa Azam utamwagiza wakala wao wa kufuatilia wachezaji wa nje ya nchini kwa ajili kwenda Ghana na Zambia kufuatiliwa wachezaji hao na iwapo ataridhishwa na mmoja kati yao basi atarudi naye kwa ajili ya kujiunga nao.


“Baada ya kuachana na straika wetu Yahya Mohamed, kocha amependekeza kati ya wachezaji wawili kutoka Ghana na Zambia ili aweze kumpata mmoja wao kwa ajili ya kuziba nafasi ya huyo aliyeondoka,”alisema.


Wakati huo huo, Jafari alisema, kikosi cha Azam kinatarajiwa kuondoka kesho kwenda Njombe kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Njombe Mji, mchezo wa raundi ya 10 wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Jumamosi hii kwenye uwanja wa Sabasaba.


Alisema, kikosi cha wachezaji 22 akiwemo na Stephane Kingue ambaye alikuwa majeruhi, kinatarajiwa kuondoka kikiwa pamoja na viongozi wa benchi za ufundi kwa ajili ya kwenda mjini humo.


“Timu inaondoka mapema kwa ajili ya kwenda kuzoea mazingira ya baridi na Njombe ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuwavaa wenyeji Njombe Mji kwenye mchezo huo,” alisema Jaffar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad