HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 19, 2017

WAZIRI UMMY MWALIMU APONGEZA WASICHANA WALIOFAULU MTIHANI WA KIDATO CHA SITA (2017)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb), anatoa pongezi za dhati, kwa wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa kidato cha Sita kwa mwaka 2017, ambapo kiwango cha ufaulu wa matokeo ya kitaifa kimepanda kwa asilimia 0.59 ikilinganishwa na mwaka 2016, huku watoto wa kike wakiongoza kwa ubora mwaka huu.

Waziri Ummy amempongeza Sophia Juma wa shule ya Sekondari Mazinde juu (Tanga) kwa kushika nafasi ya kwanza, sanjari na Agatha Julius Ninga wa shule ya Wasichana Tabora ambaye ameshika nafasi ya pili kitaifa.

Kadhalika, Waziri Ummy amewapongeza wanafunzi wote wa kike kwa jitihada walizoonesha na kuweza kufaulu mitihani yao kwa kiwango cha asilimia 97.21 ya waliofanya mtihani; ikilinganishwa na asilimia 95.34 ya wavulana waliofaulu. Waziri ameeleza kufarijika na juhudi ya wanafunzi wa kike, kufuatia ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu kupanda kwa asilimia 94.07 katika madaraja haya ikilinganishwa na wavulana waliofaulu kwa asilimia 93.49. Juhudi hizi sio za kubezwa, na ni ishara thabiti kuwa mtoto wa kike akipewa nafasi hakika anaweza.

Wizara inatambua ushirikiano wa walimu, wazazi, na jamii ambao wamewezesha kufikiwa kwa ubora wa ufaulu wa watoto wa kike. Juhudi zenu zimesaidia utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutoa fursa sawa kwa watoto wa kike na wa kiume katika kupata haki ya elimu. Mhe.Ummy amewasa watoto wa kike wa shuleni mbalimbali nchini kutafakari matokeo ya mwaka huu ili kuwa chachu ya kujitambua na kujikinga na mimba shuleni. Kama wanafunzi wa kike watajitambua watasoma kwa ari kubwa kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Niwatake watoto wote wa kike waelewe kuwa wamehitimu daraja moja, hata hivyo bado wanalojukumu la kujiendeleza zaidi katika taaluma mbalimbali kama njia ya kumwezesha mtoto wa kike na mwanamke kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa umahiri mkubwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad