HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 8, 2017

Mwenyekiti wa kijiji atekwa Ikwiriri, mwingine aokotwa mtoni amefariki kwa jeraha la risasi


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kati, Ikwiriri, Athuman Mtoteka anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.

Mwenyekiti huyo ambaye anawakilisha chama cha Wananchi CUF, anadaiwa kutekwa jana kati ya saa moja na mbili usiku.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga amesema watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake kwa miguu kisha kumchukua na kwenda naye kusikojulikana.

Amesema taarifa za tukio hilo zilitolewa katika kituo cha Polisi Ikwiriri leo Alhamisi asubuhi na mkewe.

Lyanga ameeleza kuwa baada ya kutolewa kwa taarifa hizo kituoni hapo, Polisi tayari wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya tukio hilo.

"Tumepokea taarifa hizo toka kwa mkewe akielezea mumewe kuchukuliwa na watu wasiojulikana na kuondokanae kusikojulikana" amesema Lyanga.

Kadhalika taarifa toka kwa majirani wa mwenyekiti huyo zinaeleza kuwa waliwaona watu watano waliofika nyumbani hapo wakitembea kwa miguu kisha kumkamata na kuondoka naye.

Katika tukio jingine, maiti ya mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake imekutwa ikielea ndani ya Mto Rufiji, Kitongoji cha Ngwalo kilichopo katika Kijiji cha Mtunda A, wilayani Kibiti.

Kamanda Lyanga amesema uchunguzi wa daktari juu ya maiti hiyo ulionyesha marehemu alikuwa na jeraha moja kichwani lililotokana na kupigwa risasi.

Lyanga amesema marehemu alikuwa amefungwa kamba katika mikono yake yote na maiti hiyo ilikuwa imeanza kuharibika kutokana na kukaa majini kwa muda mrefu.

Amesema kutokana na maiti hiyo kuanza kuharibika waliuruhusu uongozi wa kijiji hicho kuizika jana Jumatano.

Amesema baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliiona maiti hiyo ikielea majini kwenye mikondo ya maji ya Mto Rufiji kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji hicho nao waliotoa taarifa Polisi.

Kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Onesmo Lyanga limetoa wito kwa wananchi waishio katika wilaya za Kibiti na Rufiji kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya mauaji yanayozidi kutokea katika wilaya hizi mara kwa mara.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad