HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 21 June 2017

AGPAHI YAENDELEA KUTOA HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA KWA WATOTO NA VIJANA

Jumla ya watoto 8,615 kutoka mikoa ya Tanga, Mara, Mwanza,Geita, Simiyu na Shinyanga wamepatiwa huduma za Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ikiwemo kupatiwa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi mwezi Machi 2017. 

Huduma hizo zimetolewa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto. 

Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Miradi kutoka AGPAHI,Dk. Safila Telatela wakati wa kufungua Kambi ya Ariel 'Ariel Camp' ya siku tano inayokutanisha watoto na vijana wenye umri kuanzia miaka 10 mpaka 17 kutoka mikoa ya Shinyanga,Geita na Mwanza inayofanyika katika Hotel ya Lesa Garden jijini Mwanza. 
Mkurugenzi wa Miradi kutoka shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) Dk. Safila Telatela akizungumza wakati wa kufungua Ariel Camp (Kambi ya Ariel) ya siku tano kuanzia June 19,2017 - June 23,2017 iliyokutanisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Shinyanga,Mwanza na Geita jijini Mwanza.Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog 

Dk. Telatela alisema watoto hao ni sawa na asilimia 5 kutoka jumla ya watu 189,806 waliopatiwa huduma na shirika hilo katika kipindi hicho na shirika linaendelea na kazi ya kutoa matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 katika mikoa hiyo sita. 


Alisema pia wanafanya kazi ya kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto katika vituo 631. Aidha Dk. Telatela alisema wamefanikiwa kuunda vikundi zaidi ya 65 vya watoto na vijana katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu ambapo takribani watoto 2640 wamenufaika na vikundi hivyo. 

“Kuanzia mwezi Oktoba 2016, shirika letu limeongeza wigo wa kutoa huduma kutoka mikoa miwili ya Shinyanga na Simiyu na sasa imekuwa sita na tunafanya kazi ya kutoa matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 kwenye mikoa hii sita”,alieleza Dk. Telatela. 
Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza Dk. Pius Maselle akifungua kambi ya watoto na vijana 'Ariel Camp' katika hotel ya Lesa Garden jijini Mwanza.Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Miradi AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Gastor Njau akifuatiwa na Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Geita Dk. Joseph Odero. Wa kwanza kulia ni Mratibu wa Miradi AGPAHI mkoa wa Mwanza, Olympia Laswai akifuatiwa na Mkurugenzi wa Miradi AGPAHI, Dk. Safila Telatela. “Shirika letu limekuwa likiandaa kambi kwa ajili ya watoto na vijana kwa lengo la kuwakutanisha ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu afya, stadi za maisha, kupata ushauri wa kisaikolojia kutokana na changamoto wanazokutana nazo na pia huduma za kitabibu kutoka kwa daktari wa watoto katika kipindi chote cha kambi na kuwafanya kuwa mabalozi wa huduma za watoto katika jamii zao”,aliongeza. 

Naye Mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo, Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Pius Maselle alitoa rai kwa mikoa mipya ya AGPAHI (Geita,Tanga,Mara na Mwanza) kufanya jitihada za ziada katika uundaji wa vikundi vya watoto na vijana ili idadi ya watoto watakaonufaika na huduma za kisaikolojia iwe kubwa. 

Aidha Dk. Maselle alitoa shukrani kwa shirika la AGPAHI kwa jitihada mbalimbali linazofanya katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi nchini kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na Shirika la Development Aid From People to People (ADPP - Mozambique). 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad