HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 22 March 2017

KAMATI YA NAPE YAKABIDHI RIPOTI YA UCHUNGUZI WA UVAMIZI WA KITUO CHA CLOUDS

Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, amekabidhiwa taarifa  dhidi ya uvamizi wa kituo cha utangazaji cha Clouds na kuwashukuru kwa jitihada kubwa walizofanya bila malipo.

Waziri Nape ameipongeza kamati hiyo kwa kufanya kazi kwa uaminifu mkubwa na kuahidi Kuipeleka taarifa hiyo katika ngazi za juu na kuishukuru kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Hassan Abbas ambaye pia ni mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo.

Akipokea taarifa hiyo kutoka kwa Abbas amesema amekabidhiwa taarifa hiyo ikiwa na vielelezo vya picha za mnato (video) na sauti kwa watu waliohojiwa na amewaahidi kuwa atalifikisha mbele zaidi kwani ana wakubwa wengine ambapo yuko Waziri Mkuu, Makamu na Rais Mwenyewe, kwa hiyo kama kuna ushauri, au maelekezo wao ndio wenye mamlaka ya kusema.

 Akisoma ripoti hiyo Katibu wa kamati iliyoundwa na waziri Nape, Deodatus Balile amesema katika kukamilisha ripoti hiyo, walifanya mahojiano na wafanyakazi 14 wa kituo hicho cha radio waliokuwa zamu usiku huo.

Taarifa hiyo ya kamati ya watu watano imeeleza, ili kukamilisha taarifa hiyo walifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Mkoa bila mafanikio. "Tulimpigia simu lakini hakupokea, tulimpelekea ujumbe wa maneno lakini hakujibu, na hata tulipoenda ofisini kwake alitokea mlango wa nyuma na kuondoka." amesema Balile.

Balile ameongeza kuwa baada ya kushindwa kuonana naye, tukajiridhisha kuwa amechagua mwenyewe kutotumia fursa ya kuhojiwa. Taarifa hiyo ilieleza zaidi  kuwa katika uchunguzi wao, walijiridhisha kuwa ni kweli Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  alivamia kituo cha utangazaji cha Clouds akiwa anaendesha gari mwenyewe  akiambatana na askari wenye silaha.

Akisoma taarifa hiyo ameongeza kuwa, uchunguzi huo walioifanya umeonyesha kuwa Mkuu wa mkoa aliwatisha wafanyakazi hao na kuwalazimisha kurusha kipindi ama sivyo angewaingiza kwenye tuhuma za dawa za kulevya na kuongeza kuwa, kitendo kile kilionyesha kuwa RC aliingilia taratibu zinazofanywa na wahariri kwa kulazimisha Habari anayoitaka irushwe hewani.

Aidha akiendelea kusoma taarifa hiyo, Balile amesema kamati yao haikupata udhibitisho wowoe kuonyesha kuwa wafanyakazi walipigwa na vitako vya bunduki na kupigwa mitama. Kamati hiyo imetoa mapendekezo matatu, likiwemo la kumtaka RC aombe radhi kwa Clouds na kwa wanahabari wote kwa kuingilia Uhuru wa Habari.

Katika pendekezo lingine kamati  imewataka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi dhidi ya askari waliovamia kituo hicho kwa silaha ili waweze kuchukuliwa hatua.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari wa kupokea ripoti ya uchunguzi wa  taarifa  dhidi ya uvamizi wa kituo cha utangazaji cha Clouds baada ya tume ya saa 24 teule kuikamilisha.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akipokea ripoti ya uchunguzi wa  taarifa  dhidi ya uvamizi wa kituo cha utangazaji cha Clouds  kutoka kwa Mwenyekiti kamati hiyo Hassan Abbas ambaye pia ni mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, kulia ni katibu wa kamati hiyo teule Deodatus Balile aliyeisoma ripoti hiyo leo Jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad