HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 17, 2016

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AZINDUA KAMPENI YA KITAIFA YA KUDHIBITI MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA LEO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza kwenye viwanja vya Leaders Club.
 Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza ambapo aliwaambia wananchi walishiriki kwenye tukio hilo kuwa siri kubwa ya mafanikio yake ya kuonekana yupo imara ni mazoezi hivyo aliwataka wananchi wajenge tabia ya kushiriki na kufanya mazoezi kwani kutawaepusha na maradhi mengi .
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalim akihutubia kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi Kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza matembezi ikiwa sehemu ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi akiongozana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi (kushoto) na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalim kabla ya kufungua Kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza  kwenye viwanja vya Leaders Club viongozi wengine walioshiriki matembezi hayo ni pamoja na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalah, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda .
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja  na viongozi mbali mbali mara baada ya kufungua wa Kampeni ya Kitaifa ya Kudhibiti Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza  kwenye viwanja vya Leaders Club.

                    

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa muda wa miezi mitatu kwa Halmashauri zote nchini kurudisha serikalini haraka maeneo ya michezo yaliyovamiwa na watu kwa ajili ya kufanya shughuli zao binafsi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo baada ya kushiriki matembezi na kuzindua wa kampeni ya Kitaifa ya kudhibiti Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye viwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais ameonya kuwa kama watendaji wa mikoa na halmashauri watashindwa kurudisha maeneo hayo basi watenge haraka maeneo mengine kwa ajili ya wananchi kufanya mazoezi kama hatua ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Katika kuunga mkono utaratibu wa kufanya mazoezi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa mikoa na wilaya zote kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi angalau kwa mwezi mara Moja.

“Nitamke kuwa kila Jumamosi ya pili ya mwezi itakuwa siku ya mazoezi kwa afya kwa sababu mazoezi ni afya na nawaasa wananchi kufanya mazoezi na kuanzisha na kujiunga na vikundi vya mazoezi na serikali itatimiza wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi kote nchini”

Makamu wa Rais pia ameagiza watendaji wa Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia kurudisha mchakamchaka mashuleni kulingana na maeneo yalivyo.

Amesema mchakamchaka utasaidia kuimarisha afya za wanafunzi na kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

“Natoa rai utaratibu wa mchakamchaka katika shule zetu urudishwe mara Moja katika Muda ambao utaonekana ni mwafaka kwa shule husika”.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Afya kukamilisha haraka mchakato wa kuunda kamati ya kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza itakayojumuisha wadau kutoka wizara mbalimbali nchini.

Amesisitiza kuwa mchakato huo ni lazima ukamilike tarehe 1 machi mwaka 2017.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yanaongezeka sana duniani kote hasa kwenye nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania ambapo magonjwa hayo mpaka sasa yanachangia asilimia 27 ya vifo Duniani.

Amesema utafiti uliofanyika mwaka 2012 uliohusisha wilaya 53 hapa nchini umeonyesha viashiria hatarishi vya magonjwa hayo ambapo asilimia 26 ya wananchi ni wanene kupita kiasi,asilimia 26 wana lehemu nyingi mwilini na asilimia 25.9 wanashinikizo kubwa la damu.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta sigara na asilimia 97.2 ya wananchi wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa siku.

Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema watanzania wanaweza kukabiliana na magonjwa hayo kwa kufanya mazoezi ya viungo angalau mara tatu kwa wiki kwa muda wa nusu saa, kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa,kupunguza matumizi ya pombe kupita kiasi na kujiepusha na matumizi ya tumbaku.

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi katika nasaha zake amewahimiza Watanzania kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya zao.

Amesema kama watanzania watafanya mazoezi wataepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo,kisukari,uti wa mgongo na mifumo ya neva na figo.


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad