Mkutano wa Wakuu wa nchi na
Serikali umemalizika katika mjini Mbabane Swaziland ambapo Tanzania imeteuliwa
kuwa Mwenyekiti wa Asasi muhimu na nyeti ya Siasa, Ulinzi na USalama ya Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika- SADC- (SADC
Organ On Politisc, Defence and Security Cooperation) ambapo nchi ya Angola
imeteuliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa asasi hiyo.
Jukumu kubwa la asasi hiyo litakuwa
ni kuangalia masuala yote yanahusiana na Siasa, ulinzi na usalama katika ukanda
wa SADC huku changamoto kubwa ikiwa ni namna ya kutafuta suluhu ya kudumu
hususani katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na
Lesotho.
Akizungumzia mambo muhimu
yaliyojiri kwenye Mkutano huo wa 36 wa SADC mjini Mbabane - Swaziland, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye alimwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli amesema mkutano huo umekuwa
wa mafanikio makubwa na amehimiza ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama katika
kuwaletea wananchi maendeleo.
Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan amesema kuwa nchi wanachama wa SADC kwa sasa zinatakiwa kuongeza juhudi
katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuzitafutia
ufumbuzi haraka kama hatua ya kujenga ustawi bora wa wananchi wa kanda hiyo.
Kuhusu Mpango wa Mfalme wa
Swaziland wa III wa kujenga Chuo Kikuu cha SADC nchini mwake kabla ya mkutano ujao
wa SADC hapo mwakani chuo ambacho kwa kuanzia kitatoa ufadhili wa masomo ya
Sayansi,Ugunduzi na Utafiti kwa wanafunzi wanaotoka kwenye nchi wanachama wa
SADC, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema mpango huo ni mzuri na
utasaidia kutoa wataalamu wengi hasa wanasayansi katika ukanda wa SADC na
serikali ya Tanzania inaunga mkono mkakati huo.
Kuhusu Tanzania kuteuliwa
kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa nchi za SADC, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa Dkt
Augustine Mahiga amesema Tanzania itahudumu katika asasi hiyo kwa mwaka MMOJA
na anaimani kuwa changamoto za kisiasa zilizopo katika nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Lesotho zipatiwa ufumbuzi.
Mkutano wa wakuu wa nchi na
serikali wa SADC pia umeiteua nchi ya Swaziland kuwa mwenyekiti wa SADC na
Jamhuri ya Afrika Kusini imeteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC.
Katika mkutano huo wakuu wa
nchi na serikali wametia saini rasimu
za maboresho ya mikataba mbalimbali
ya jumuiya hiyo ikiwemo mkataba wa
kuboresha itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya itifaki ya ushirikiano
wa siasa, ulinzi na usalama ya SADC na maboresho ya itifaki ya biashara.
Imetolewa
na
Ofisi
ya Makamu wa Rais
Mbabane
Swaziland
1-Sep-16
No comments:
Post a Comment