HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 4, 2016

Mwijage atembelea eneo la viwanda Tundwi Songani, wilaya ya Kigamboni

Watanzania wameshauriwa kupenda bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini ili kusaidia kukuza biashara na kuunga mkono juhudi za serikali za kutaka kujenga nchi ya viwanda. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage alisema hayo wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Milkcom Dairies Limited kilichopo eneo la Kibada wilaya ya Kigamboni mwishoni mwa wiki. 
 “Tukipenda bidhaa zetu tunatengeneza soko kwa viwanda vyetu kuzalisha zaidi, kukua na kujenga uchumi wetu,” alisema. Alisifu juhudi zinazofanywa na kiwanda hicho kinachozalisha maziwa kwa jina la Dar Fresh na bidhaa nyingine za maziwa, na maji ya chupa. Pia kiwanda hicho kiko katika harakati za kuanza kuzalisha vinywaji baridi na kukamua matunda kwa ajili ya kutengeneza juisi mbalimbali. 
 “Nimefurahishwa na kazi yenu, mnafanya vizuri,” alisema. Kiwanda hicho chenye n’gombe wa maziwa 3,000 kinazalisha wastani wa lita 10,000 za maziwa kila siku. Pia kinakusanya maziwa toka kwa wafugaji hasa kutoka maeneo ya mkoa wa Morogoro na Pwani kama Dakawa, Kimamba, Lugoba na Chalinze. Mkurugenzi wa maziwa ya Dar Fresh, Bw. Yusuph Said alisema utaratibu huo umesaidia kutengeneza soko la uhakika kwa wafugaji hao.
 “Tunakusanya wastani wa lita 8,000 kila baada ya siku moja toka kwa wakulima hao,” alisema Bw. Said. Waziri aliuahidi uongozi wa kiwanda hicho kufuatilia kwa karibu ili kupata umeme wa uhakika kutoka gridi ya taifa na miundombinu mingine ya muhimu ili waweze kuwa washindani zaidi. Kampuni ya Milkcom Dairies Limited iko chini ya umoja wa makampuni ya Oilcom. Katika ziara hiyo, 
Waziri Mwijage pia alitembelea eneo la mradi wa viwanja 240 vilivyotengwa na serikali katika eneo la Tundwi Songani, Kigamboni kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na viwanja 100 vya makazi kwa watakaokuwa wanaendesha viwanda hivyo. Alisema kazi kubwa ya serikali baada ya kupima viwanja hivyo ni kuhakikisha kuwa panakuwa na umeme wa uhakika, maji, barabara na miundombinu mingine ili kuvutia wawekezaji. 
 “Tuangalie jinsi ya kuvuta bomba la gesi eneo hili ili kuvutia wawekezaji haraka,” aliwaambia maafisa wa serikali aliofuatana nao. Alisema atahakikisha kuwa eneo hilo linapata miundombinu inayotakiwa ndani ya miaka miwili kuanzia sasa ili wawekezaji katika sekta ya viwanda wafanye kazi zao bila matatizo. 
 Pia alisisitiza utunzaji wa mazingira kwa wenye viwanda. Mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Bw.Hashim Mgandilwa alisema wilaya yake imejipanga kuhakikisha maeneo hayo yanatumika kama ilivyopangwa na serikali. “Tunahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hapa kwa faida ya pande zote mbili,” alisema. Kamishna wa Ardhi Msaidizi, Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Mathew Nhonge alisema maeneo hayo ni kwa ajili ya viwanda vidogo na viwanda vya kati.
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage (wa pili kushoto) akifuatilia maelezo wakati wa ziara yake katika kiwanda kinachozalisha bidhaa za maziwa kilicho chini ya Milkcom Dairies Limited eneo la Kibada wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki.  Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa makampuni ya Oilcom, Bw. Said Nahdi na Mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Bw. Hashim Mgandilwa (kushoto).
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage (kushoto) akifuatilia maelezo wakati wa ziara yake katika kiwanda kinachozalisha bidhaa za maziwa kilicho chini ya Milkcom Dairies Limited eneo la Kibada wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki. Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa makampuni ya Oilcom Group, Bw. Said Nahdi na Mkurugenzi wa maziwa ya Dar Fresh, Bw. Yusuph Said (kulia).
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage (kulia) akisisitiza jambo alipokuwa akipewa maelezo wakati wa ziara yake katika eneo la viwanja 240 vilivyotengwa kwa ajili ya viwanda katika eneo la Tundwi Songani, wilaya ya Kigamboni mwishoni mwa wiki.  
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage (katikati) akifuatilia maelezo wakati wa ziara yake katika kiwanda kinachozalisha bidhaa za maziwa kilicho chini ya Milkcom Dairies Limited eneo la Kibada wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki.  Kushoto ni Mkurugenzi wa makampuni ya Oilcom, Bw. Said Nahdi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad