Mtoto Aisha Mshantu (kulia )akimkabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme aliyoyatoa katika shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma.
NA RAMADHANI JUMA, DODOMA
KATIKA hali isiyotegemewa msichana mdogo Aisha Mshantu ambaye ni muhitimu wa kidato cha sita mwaka 2016 ameitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli wa kuwaomba wadau kushiriki katika zoezi la kuchangia madawati kwa ajili ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari nchini ili waondokane na adha ya kujifunza wakiwa wameketi chini.
Aisha ametoa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2 katika shule ya Msingi ya Mwenge iliyopo katika kijiji cha Mbabala A Kata ya Mbabala Manispaa ya Dodoma, ambapo amesema hiyo ni ndoto yake ya muda mrefu na kwamba anafuraha kuikamilisha ili kuonesha alivyoguswa na tatizo la wanafunzi kukaa chini wakati wa kujifunza.
Mtoto
Aisha Mshantu na wazazi wake Mzee Mshantu (wa kwanza kulia) na Bi
Rehema (wa pili kulia) wakiwa amekaa katika madawati aliyoyatoa mtoto
huyo kama msaada katika shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Mbabala
Manispaa ya Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina
Mndeme.
Mbali na msaada huo wa madawati, msichana huyo ambaye amezaliwa akiwa mlemavu, pia ametoa msaada wa mataulo maalum 84 kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika shule hiyo yenye thamani ya shilingi laki mbili, kama chachu ya kuwazindua wasijiingize katika masuala ya mahusiano kwa kudanganywa na wanaume kwa kuahidiwa mahitaji madogo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni hapo juzi baada ya kupokea misaada hiyo kwa niaba ya Serikali na Manispaa ya Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme alimshukuru mtoto Aisha kwa msaada huo ambapo alisema msichana huyo ameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa watoto wenzake huku akitoa wito kwa jamii kujifunza kutokana na tukio hilo.
“Hakuna fedha isiyokuwa na kazi..Aisha ana mahitaji yake na angeweza kuzitumia fedha hizi kwa matumizi mengine ya binafsi lakini yeye ameamua kusaidia wadogo zake wa shule ya Msingi..hili ni jambo la kijasiri sana kwa mschana mdogo kama huyu na ni funzo kubwa kwa jamii nzima” alisema.
Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kushoto) akimshukuru mtoto Aisha
Mshantu kwa Msaada wa madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.2
aliyoyatoa katika shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Mbabala
Manispaa ya Dodoma.
Akielezea ndoto aliyokuwa nayo mtoto wake kwa muda mrefu, mama mzazi wa Aisha Bi Rehema alisema mtoto wake huyo alifungua akaunti ya ‘Jumbo Junior’ katika Benki ya CRDB Dodoma na kuanza kujiwekea akiba kidogo kidogo hadi alipofikia azima yake hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Felister Bura ameahidi kukarabati darasa moja katika shule hiyo ambako madawati hayo yatatumika, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Msichana Aisha ambaye kwa sasa ni Balozi wa Elimu wa Umoja wa Mataifa (UN) kupitia programu ya ‘4 Quality Education’.

No comments:
Post a Comment