HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 27, 2015

Benki ya Afrika(BOA Bank) yapigia chapuo matumizi bora ya mikopo

Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
WATANZANIA wametakiwa kujenga tabia ya kukopa na kurejesha kwa wakati mikopo katika taasisi za fedha kwani huo ni msingi muhimu wa kujipatia maendeleo kwa mtu binafsi na katika ngazi ya taasisi pia.

Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Afrika, Bw. Mussa Mwachaga amesema mwishoni mwa juma wakati akikabidhi msaada wa Tsh. milioni 10 kwa shule ya Sekondari ya Baobab kuwa uaminifu katika kurejesha mikopo huleta maendeleo ya haraka kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali.

“Hili ni wazi, wale wanaojenga uaminifu na taasisi za fedha hufanikiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema.

Alisema uongozi wa shule hiyo ya sekondari ni mfano hai wa taasisi zilizojijengea uaminifu mkubwa wa kurejesha mkopo na sasa imejijengea mahusiano mazuri ya kuendelea kukopa zaidi na kufikia malengo yake.

Msaada huo ni sehemu ya ahadi ya Tshs milioni 40 zilizoahidiwa na benki kwa shule hiyo.

Pesa hizo zitatumika katika ukarabati wa bweni la wasichana ambalo nalo lilijengwa mwaka 2006 kwa mikopo toka benki hiyo.

Mkurugenzi na mmiliki wa shule hiyo, Bw. Halfan Swai aliipongeza benki hiyo kwa kuamua kumpatia msaada huo ambao utatolewa kwa awamu kwa jili ya ukarabati wa majengo ya shule.

“Kwa vile jengo hili lilijengwa kwa mkopo wao, leo nimewapa fursa ya kulizindua rasmi,” alisema na kuongeza kuwa kwa heshima ya benki hiyo bweni litapewa jina la ‘Bweni la Benki ya Afrika.’

Alisema benki hiyo imeisaidia shule yake na kuwa hadi ilipofikia imeshapata mkopo zaidi ya Tshs bilioni 2.

Alifafanua kwamba siri ya kuendeleza mahusiano na benki ni kurejesha mikopo kwa wakati sababu bila hivyo haiwezekani kuendelea kukopa.

Meneja wa shule hiyo, Bi. Sophia Mawenya alisema bweni linalokarabatiwa linachukua wanafunzi 408 ambapo kila chumba kina uwezo wa wanafunzi nane.

“Tunahitaji benki hii iendelee na ushirikiano huu kwa vile malengo yetu ya kujenga shule ya msingi na chuo kikuu bado hayajafikiwa,” alisema.

Alisema malengo hayo yatafikiwa tu kwa kukopa fedha katika taasisi za fedha kama Benki ya Afrika.

Katika tukio hilo, wafanyakazi wa benki hiyo walishiriki katika kazi ya kupaka rangi bweni  hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad